Israel yashambulia Hezbollah, Lebanon

Jeshi la Israel, Jumapili limesema ndege zake za kivita zilishambulia maeneo ya Hezbollah mashariki mwa Lebanon, ambako kundi hilo linaloungwa mkono na Iran, lina uwepo mkubwa kulipiza kisasi kwa kutunguliwa moja ya ndege zake zisizo na rubani.

Chanzo kilicho karibu na Hezbollah, kilimwambia mwandishi wa AFP katika eneo la Baalbek, mashariki mwa Lebanon kwamba mashambulizi hayo yalilenga Janta, na Sifri, katika bonde la Bekaa, karibu kilomita 80 kutoka mpaka wa karibu wa Israel.

Jeshi la Israel limesema kwenye Telegram, kwamba ndege za kivita zilishambulia kambi ya kijeshi na maeneo mengine matatu ya miundombinu ya kigaidi ya mtandao wa ulinzi wa anga wa Hezbollah katika eneo hilo.

Limesema mashambulizi hayo yalikuwa ya kulipiza kisasi ambapo ndege isiyo na rubani ya jeshi ilitunguliwa na kombora la kutoka ardhini hadi angani Jumamosi. Taarifa kutoka idara ya ulinzi wa raia ya Lebanon imesema hakuna aliyejeruhiwa.