Israel yaokoa watu wanne miongoni mwa waliotekwa nyara na Hamas

  • VOA News

Mtu akitembea karibu na picha za watu waliotekwa na Hamas Oktoba 7. Tel Aviv, Mei 31, 2024.

Israel imesema Jumamosi kwamba imewaokoa watu wanne miongoni mwa wale waliotekwa nyara wakati wa shambulizi la Hamas la Oktoba 7, ikisemekana kuwa operesheni kubwa zaidi ya uokozi tangu kuanza kwa vita vya Hamas huko Gaza.

Jeshi la lsrael limesema kuwa limewaokoa Noa Argamani, mwenye umri wa miaka 25, Almog Meir Jan, wa umri wa miaka 21, Andrey Kozloz, miaka 27, na Shlomi Ziv, mwenye umri wa miaka 40, kwenye operesheni ya mchana mjini Nuseirat.

Kundi la Hamas lilliwachukua mateka takriban watu 250 wakati wa shambulizi lao, suala lililopelekea mapigano yanayoendelea kati yake na Israel. Takriban nusu yao waliachiliwa wakati wa sitisho la mapigano la wiki moja hapo Novemba, wakati Israel ikisema kuwa zaidi ya 130 bado wanashikiliwa, robo yao wakiaminika kuwa wamekufa.

Uokozi wa Jumamosi umefanyika wakati kukiwa na shinikizo la kimataifa dhidi ya Israel, la kupunguza umwagikaji wa damu kwenye vita vya Gaza ambavyo vimefikisha miezi 8 wiki hii. Ikiwa kama juhudi ya kukwamua mazungumzo yaliokwama ya sitisho la mapigano kati ya Israel na Hamas, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amepanga kufanya zaira ya Mashariki ya Kati wiki hii.