Israel yafuta vibali kwa waandishi wa habari wa Al Jazeera

  • VOA News

Picha hii inaonyesha ofisi ya Al Jazeera mjini Jerusalem. Picha ya AP

Israel Alhamisi ilitangaza kwamba imefuta vibali vya uandishi wa habari kwa wanahabari wanne wa Al Jazeera wanaofanya kazi ndani ya nchi.

“Hiki ni chombo cha habari ambacho kinasambaza maudhui ya uongo, ikiwemo uchochezi dhidi ya Waisrael na Wayahudi na ni tishio kwa wanajeshi wa IDF,” mkurugenzi wa ofisi ya vyombo vya habari vya serikali Nitzan Chen alisema katika taarifa.

Waandishi wa habari nchini Israel hawatakiwi kuwa na kadi ya ofisi ya vyombo vya habari vya serikali, lakini ni vigumu kufika bungeni au kwenye wizara za serikali bila kadi hiyo.

Taarifa hiyo ilisema matumizi ya kadi hizo na waandishi wa habari yanaweza “kuhatarisha usalama wa serikali wakati huu wa dharura ya kijeshi.”

Agizo hilo litatekelezwa kwa waandishi wa habari wanne wa Al Jazeera ambao aidha ni raia wa Israel au wakazi wa Palestina wa Jerusalem mashariki inayokaliwa, kulingana na shirika la habari la AFP.

Al Jazeera haikujibu mara moja ombi la VOA kutoa maelezo. Lakini Walid Omary, mkuu wa ofisi ya Al Jazeera katika maeneo ya Wapalestina, aliiambia AFP kwamba serikali ya Israel ilikuwa haijawafamisha rasmi kwa maandiko uamuzi huo.