Israel yaendelea kushambulia Lebanon

Vikosi vya Israel vilifanya mashambulizi kadhaa makubwa ya anga Alhamisi kulenga vitongoji vya kusini mwa Beirut, siku moja baada ya kufanya mashambulizi makubwa mashariki na kusini mwa Lebanon, na kuua watu 52 na kujeruhi wengine 161, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Lebanon.

Mashambulizi ya Alhamisi yalijumuisha yale ya karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Lebanon, ambayo yalifanyika baada ya jeshi la Israeli kutoa agizo la watu kuondoka eneo hilo.

Jeshi la Israel limesema lilifanya mashambulizi ya anga dhidi ya makao makuu ya Hezbollah na miundombinu yao ya kijeshi ya Beirut.

Alhamisi pia, Umoja wa Mataifa umesema walinda amani wake watano walijeruhiwa baada ya msafara wao katika mji wa kusini wa Sidon ulikaribia kwenye shambulizi la ndege zisizo na rubani.

Umoja wa Mataifa haukusema kama ndege isiyo na rubani ilikuwa ya Israel au Hezbollah.