Jeshi la Israel limesema kwamba limetekeleza mashambulizi ya anga kaskazini na kusini mwa Gaza, siku moja baada ya Marekani kupiga kura ya turufu dhidi ya azimio la baraza la usalama la umoja wa mataifa , kutaka kusitishwa haraka kwa vita kwa misingi ya kibinadamu.
Jeshi la Ulinzi la Israel limeripoti kuua darzeni ya wanamgambo, ikiwemo katika eneo la Khan Younis, kusini mwa ukanda wa Gaza.
Wizara ya afya inayosimamiwa na kundi la Hamas huko Gaza, imesema leo Jumatano kwamba imerekodi vifo 118 katika siku moja iliyopita, na hivyo kufikisha idadi ya wapalestina waliouawa kufikia 29,313 na 69,333 kujeruhiwa tangu vita vilipoanza mwezi Oktoba.
Kwa wiki kadhaa, Marekani, Misri, Qatar na Israel zimekuwa zikifanya mazungumzo yenye lengo la kuachiliwa huru mateka wote na kuongeza muda wa sitisho la mapigano.