Iran imefungua kwa haraka mitambo ya ziada ya kurutubisha madini ya uranium kwenye eneo lake la Fordow na kuanza kuweka mingine, ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya nguvu za nyuklia IAEA imesema.
Hali hiyo imetokana katika kile wanadiplomasia walichoeleza kuwa ni kulipiza kisasi azimio la bodi ya shirika hilo.
Reuters Jumatano iliripoti kwamba wanadiplomasia wamesema Iran, imejibu azimio la bodi ya shirika la kimataifa la nguvu za atomiki dhidi yake wiki iliyopita kwa kupanua uwezo wake wa kuongeza uranium katika maeneo yake mawili ya chini ya ardhi ya Fordow na Natanz, lakini ongezeko hilo sio kubwa kama wengi walivyohofia.
Ripoti ya siri ya IAEA iliyotumwa kwa nchi wanachama ilieleza hatua ambazo Iran imechukua hadi sasa, huku hatua madhubuti pekee hadi sasa katika mojawapo ya maeneo yake zimechukuliwa huko Fordow, ambayo imechimbwa kwenye mlima.