Iran imemuhukumu kifo afisa mkuu wa zamani wa ulinzi baada kumkuta na hatia kwa mashtaka ya kuifanyia ujasusi Uingereza, chombo cha habari chenye uhusiano na serikali kimeripoti Jumatano.
Mahakama imesema Ali Reza Akbari, ambaye alikuwa naibu waziri wa ulinzi hadi mwaka 2001, alikuwa “jasusi mkuu” wa idara ya ujasusi ya Uingereza, shirika la habari la Tasmin limeripoti.
Tasmin imeripoti pia kuwa alifanya ujasusi kwenye mazungumzo ya zamani ya nyuklia kati ya Iran na mataifa ya magharibi.
Akbari alihudumu kama naibu waziri wa ulinzi chini ya uongozi wa Rais Mohammad Khatami, mwanamageuzi ambaye alishinikiza kuboreshwa kwa uhusiano na nchi za magharibi.
Uingereza imeomba hukumu hiyo isitishwe na Akbari aachiliwe mara moja.
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza James Cleverly amesema katika taarifa “ Hiki ni kitendo kilichochochewa kisiasa na utawala wa kikatili ambao unapuuza kabisa maisha ya binadamu.”