Maafisa ujasusi wa Marekani, Jumatatu wamesema wana uhakika Iran ilihusika na udukuzi wa kampeni ya urais ya Donald Trump, wakielezea tukio hilo kama sehemu ya juhudi kubwa na pana za Tehran kuingilia siasa za Marekani na kudhoofisha imani katika taasisi za kidemokrasia.
Ingawa kampeni ya Trump na wachunguzi wa usalama wa mitandao wa sekta ya binafsi hapo awali walisema Iran ilihusika na majaribio ya udukuzi, ikiwa ni mara ya kwanza kwa serikali ya Marekani kulaumu kufanyika shambulizi kama hilo.
Taarifa ya pamoja kutoka kwa FBI na mashirika mengine ya serekali kuu pia yameonyesha Iran inahusika na majaribio ya kudukua kampeni ya Makamu wa Rais Kamala Harris, ikisema wadukuzi waliwafikia watu walio karibu na kampeni za urais za vyama vyote viwili.
Lengo la udukuzi na mengineyo, maafisa wanasema haikuwa tu kuzusha mifarakano bali pia kuweka ushawishi katika matokeo ya uchaguzi.