Iran inasema imedhibiti mabomu 30 yaliyokusudiwa kulipuka mjini Teheran

Rais wa Iran Ebrahim Raisi

Mamlaka nchini Iran zimedhibiti mabomu 30 yaliyokusudiwa kulipuka kwa wakati mmoja mjni Teheran na kuwaweka kizuizini magaidi 28 wanaohusishwa na kundi la Islamic State, shirika la habari la Iran Tasmin limeripoti Jumapili, likinuku wizara ya ujasusi.

“Baadhi ya wanamgambo hao ni wa kundi la Islamic State na wahusika wana historia ya kujiunga na makundi ya Takfiri nchini Syria, Afghanistan, Pakistan na eneo la Kurdistan la Iraq,” wizara ya ujasusi iliongeza katika taarifa.

Kundi la Islamic State lilidai kufanya mashambulizi kadhaa nchini Iran, yakiwemo mashambulizi mawili mabaya mwaka 2017 ambayo yalilenga bunge la Iran na kaburi la mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, Ayatollah Ruhollah Khomeini.

Hivi karibuni, Islamic State ilidai kuhusika na shambulio kwenye nyumba ya ibada ya Washia Oktoba mwaka jana, ambapo watu 15 waliuawa kusini magharibi mwa Shiraz.