Iran imeapa kulipiza kisasi kutokana na shambulizi la Islamic State

Shambulizi hatika hekalu takatifu la Shah Cheragh Shrine mjini Shiraz, Iran Okt 26, 2022

Iran imesema kwamba italipiza kisasi shambulizi lililotekelezwa dhidi ya hekalu takatifu na kupelekea vifo vya watu 15.

Kundi la wapiganaji wa kiislamu la Islamic State limedai kutekeleza shambulizi hilo.

Shambulizi hilo linaongeza shinkizo dhidi ya serikali inayokabiliwa na maandamano kutoka kila sehemu ya nchi kufuatia kifo cha Mahsa Amini, mwanamke mwenye umri wa miaka 22 mwenye asili ya kikurdi, aliyefariki dunia akiwa mikononi mwa polisi, Septemba 16.

Kamanda wa kikosi maalum cha kijeshi cha Iran Hossein Salami, amesema kwamba moto wa kulipiza kisasi utawafikia waliotekeleza shambulizi hilo.

Maafisa wa Iran wamesema kwamba wamewakamata mtu aliyekuwa na bunduki, aliyetekeleza shambulizi hilo katika sehemu takatifu ya kuabudu ya Cheragh, mjini Shiraz.

Mauaji hayo ya mahujaji wa wakishia, yamefanyika siku ambayo maafisa wa usalama wa Iran walikabiliana na waandamanaji waliojitokeza kuadhimisha siku 40 tangu kifo cha Amini.

Kundi la kutetea haki za kibinadamu la Hengaw limesema kwamba vijana wawili walipigwa risasi na kuuawa wakati wa maandamano hayo katika mji mkuu wa mkoa wa Kikurdi, Sanandaj.