IOM yatoa ripoti mpya ya vifo vya wahamiaji Mediterrannean

Boti iliyojaa wahamiaji katika Mediterrannean wakipatiwa msaada kutoka boti ya uokozi

Ripoti mpya ya shirika la kimataifa la wahamiaji-IOM imegundua kwamba takriban wahamiaji 60,000 wamekufa au kupotea kwenye bahari au njia za ardhini mnamo miongo miwili iliyopita. IOM inachukulia kwamba idadi kamili huwenda ikawa kubwa zaidi kwa sababu miili mingi bado haijapatikana au kutambuliwa.

Ripoti inaeleza kwamba vifo vingi vilivyojulikana katika kipindi cha miaka milili iliyopita vimetokea katika kanda ya Mediterranean. Shirika la kimataifa la wahamiaji-IOM linakadiria wahamiaji 5,400 duniani wamekufa au wamerikodiwa kuwa wamepotea katika mwaka 2015.

Mwaka huu, IOM imeorodhesha zaidi ya vifo vya wahamiaji 3,400 duniani kote. Mkurugenzi wa kitengo cha uchambuzi wa takwimu wa IOM, Frank Laczko anasema zaidi ya asilimia 80 ya vifo vilikuwa vya watu wanaojaribu kufika ulaya kwa njia ya bahari.

Shirika la kimataifa la wahamiaji-IOM

Anasema mtu mmoja kati ya watu 23 ambao wamejaribu kuvuka kupitia kati kati ya bahari ya Mediterrannean wamekufa au hawajumuishwi miongoni mwa wahamiaji mwaka huu, jambo ambalo ni la kusikitisha.

Mkataba kati ya Uturuki na ulaya uliolenga kuwapa wahamiaji njia halali kuelekea ulaya kwa kiasi kikubwa umefunga njia ya mashariki mwa bahari ya mediterrannean kutoka Uturuki kuelekea Ugiriki. Hivyo basi wahamiaji wengi wanahatarisha maisha yao kwa kufuata njia ya hatari Zaidi kutokea Libya kwenda Italy.