Shirika la kimataifa la uhamiaji IOM, linaeleza kuwa litazidisha kurudishwa makwao wahamiaji wa Kiafrika wanaoathirika manyanyaso na ukandamizaji nchini Libya, hususan mikononi mwa polisi na wanamgambo.
Katika kipindi cha miezi michache iliyopita, shirika la IOM linaripoti kuwa limerudisha makwao maelfu ya waafrika kutoka Libya, hususan kutoka Burkina Faso, Gambia na Senegal. Katika operesheni yake ilofanyika hivi karibuni, IOM ilirudisha wahamiaji 117 nchini Burkina Faso, ikiwa ni pamoja na wanawake 5 na watoto 2.
Msemaji wa IOM Itayi Viriri, alisema wahamiaji hueleza hadithi za manyanyaso mabaya yanayofanywa na wanamgambo, na kwenye ajira zao. Anasema vijana wengi wa kiume wanazungumzia kufanya kazi kwa mda mrefu bila ya malipo.
Bw. Viriri anasema kuwa , wana mifano ya vijana wakiume ambao walikuwa wakifanya kazi za ujenzi, na ambao kila wanapolipwa mishahara yao, basi huvamiwa kwenye makazi yao na wanamgambo ambao huchukuwa pesa zote walokuwa nazo. Hawakuwa na mahala pa kwenda kujaribu kupata msaada au uhalifu huo kuchunguzwa.
Ripoti ya hivi karibuni ya umoja mataifa imegundua kuwa wahamiaji nchini Libya wako katika mazingira hatari ya kunyanyaswa na kukumbwa na ukiukaji wa haki za binadam unaofanywa na mamlaka za huko, makundi yenye silaha na walanguzi. Ripoti inaeleza kuwa wahamiaji wengi wamekumbana na vipindi virefu vya kufungwa kiholela, kuteswa, kulazimishawa kufanya kazi, ulafi, na aina nyengine za manyanyaso.
Viriri ameiambia voa kuwa IOM ilipokea ushuhuda kutoka kwa wahamiaji wakiafrika kuwa wanapigwa na kutishwa na aina mbalimbali za adhabu za kinyama.
Viriri anasema kwamba, kuna kesi kadhaa ambapo watu walitekwa nyara kwa matarajio kuwa watalipwa fidia. Kwa hivyo, tuna kijana mmoja amabye alisema kuwa wakikamatwa nchini Libya, au kutekwa na wanamgambo hao, basi wanatarajiwa kulipa takriban dola mia 7.
Viriri anasema wahamiaji wengi waloondolewa kutoka Libya katika kipindi cha mwaka ulopita, na wahamiaji wapya. Anasema wanakuja wenyewe kwenye ofisi za IOM wakiomba msaada kurejea nyumbani kwa sababau hawawezi tena kuhimili maisha nchini Libya.