Ikulu -Kenya yatoa maelezo kuhusu mawaziri

Rais Uhuru Kenyatta

Ikulu ya Rais Kenyatta, nchini Kenya imefafanua kuwa mawaziri wote wataendelea kushikilia wadhifa wao mpaka pale Rais Uhuru Kenyatta atapokamilisha kupanga timu yake mpya itayofanya kazi naye katika awamu ya pili ya uongozi wake.

Katika tamko alilolitoa msemaji wa ikulu hiyo Manoah Esipisu, Jumamosi, amesema shauri hili liko sambamba na waraka uliotolewa na mkuu wa utumishi wa umma Disemba 2017.

“Katika siku zijazo, Mheshimiwa Rais atamaliza jukumu lake la kupanga baraza lake la mawaziri ili kutumikia awamu ya pili ya uongozi wake, akiongozwa na sifa, uaminifu, na uwajibikaji kwa kufuata Katiba.

Siku ya Ijumaa Rais Kenyatta alitangaza wateule tisa katika baraza lake la mawaziri jipya, akiwatema baadhi ya mawaziri waliokuwa wanatumikia katika serikali yake.

Mbali na wanawake watano ambao hawako katika idadi ya mawaziri tisa waliotangazwa, wengine walioachwa ni waziri wa michezo Hassan Wario, waziri wa ugatuzi Mwangi Kiunjuri, waziri wa ardhi Jacob Kaimenyi, waziri wa maji Eugene Wamalwa, waziri wa kilimo Willy Bett, waziri wa madini Dan Kazungu, waziri wa viwanda Adan Mohamed na waziri wa afya Cleopa Mailu.

“Nitaendelea kutangaza waliochaguliwa katika nafasi za uwaziri zilizobakia na nafasi nyinginezo za makatibu wakuu na wakuu wa mashirika ya umma wakati tukiendelea kuwaweka wale wachapakazi katika serikali yetu ambao watatekeleza ajenda ya miaka mitano ijayo,” amesema Kenyatta.