Mpaka Jumamosi vyombo vya habari nchini Kenya vimeripoti kuwa kuna ugomvi juu ya tenda ya Shs bilioni 2.5 iliyotolewa kwa kampuni ya Dubai ambayo imeleta vita kubwa kati yake na mawakala wa uchapishaji ikiwa ni dalili ya wasiwasi mkubwa unaoikabili tume hiyo.
Katika maadalizi ya uchaguzi wa mwaka huu, Tume ya uchaguzi hiyo imepuuzia msukumo uliokuwepo dhidi ya kuipa tenda kampuni ya Al Ghurair ya Dubai ambayo tayari imeagizwa kutengeneza karatasi za kura zaidi ya milioni 130.
Hili limefanyika baada ya tume kushindwa mara mbili kukamilisha mchakato wa kutoa mkataba huo, mara baada ya mahakama kuu kufutilia mbali tenda iliyopitishwa hapo awali.
Mwezi Aprili, IEBC ilikabiliwa na hali kama hiyo ambapo ililazimika kusitisha mpango wa Shs bilioni 3.8 uliokubaliana na kampuni ya Integrated Elections Management System (KIEMS), ikisema kulikuwa na mapambano kati ya wanaowania tenda hiyo.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Tume Wafula Chebukati ameeleza wazi na kuonya kuwa tume haitokubali kushinikizwa na kampuni au mtu yoyote ambaye anashiriki katika “vita ya tenda hizi”.
Amedai kuwa ikiwa shinikizo hili ni kwa ajili ya kuharibu uchaguzi wa kweli, haki na huru na kusema kuwa inaridhisha kuwa na kampuni mmoja itakayo tengeneza karatasi za kura ili kuondoa wale mawakala wanaotaka kudhoofisha uchaguzi.
“Kuna mawakala wanapigania tenda huko. Tume haiwezi kuruhusu vita za mawakala hawa na watu binafsi waharibu mchakato wetu wa uchaguzi. Ndio maana tunafuta tenda zote,” Chebukati alisema Aprili
Na mnamo mwaka 2012, IEBC ilishindwa kukamilisha tenda ya Shs bilioni 3.9 kwa kuagiza teknolojia iliyotumika katika uchaguzi wa mwaka 2013 Kenya, ilipelekea serikali kufikia makubaliano na Canada.