IEBC: Makamishna 4 waliotofautiana na mwenyekiti walitumiwa kisiasa ili kuvuruga matokeo

Makamishana 4 wa IEBC waliojitenga na matokeo ya kura za urais, wakiongozwa na naibu mwenyekiti wa tume hiyo Juliana Cherera ( anayeonekana kuzungumza) wakihutubia waandishi wa habari Agosti 15 2022

Wakili wa tume huru ya uchaguzi na mipaka ya Kenya IEBC Githu Muigai, ameiambia mahakama ya juu inayosikiliza kesi ya uchaguzi wa urais kwamba makamishna 4 wa tume hiyo ya uchaguzi walitumiwa kuchafua utendakazi wa tume na kutaka watu kukosa imani na matokeo ya uchaguzi.

Muigai ameiambia mahakama kwamba makamishna Juliana Cherera ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa tume ya IEBC, Irene Masit, Francis Wanderi na Justus Nyang’aya walitumiwa na watu walio nje ya tume hiyo waliotaka zoezi la kutangaza mshindi wa uchaguzi kutomalizika.

Amesema kwamba hilo lilidhihirisha pale ilipobainika kwamba Dr. William Ruto alikuwa anaongoza katika hesabu ya kura za urais, mbele ya Raila Odinga.

“Hatua ya makamishna hao kujiondoa katika shughuli ya kumtangaza mshindi wa urais wakati zoezi lilikuwa linaelekea kukamilika, ulikuwa uamuzi uliofanywa baada ya kujua mshindi”, amesema Muigai akiongezea kwamba “kulikuwa na nguvu za nje ya tume ya uchaguzi kuhakikisha kwamba zoezi la kujumlisha na kuhakiki hesabu ya kura za urais halikamiliki na mshindi asitangazwe”.

Prof Muigai amesema kwamba iwapo mshindi wa urais asingetangazwa, Kenya ingeingia katika mgogoro mkubwa wa kikatiba.

Makamishna wa IEBC wanaomulikwa

Makamishna Cherera, Wanderi, Nyang’aya na Masit waliondoka kwenye ukumbe wa Bomas, ambapo shughuli ya uhakiki na kutangazwa kwa matokeo ya kura za urais ilikuwa inaelekea kukamilika, mnamo Agosti 15 2022.

Walizungumza na waandishi wa habari katika hoteli moja katikati mwa jiji la Nairobi.

Walifanya hivyo muda mfupi kabla ya mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Wafula Chebukati kutangaza matokeo ya kura za urais.

Walidai kwamba mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Chebukati alikuwa amewatenga katika shughuli nzima ya kujumulisha matokeo ya kura hizo.

Walimshutumu Chebukati wakidai kwamba “alikuwa akijumlisha matokeo katika mazingira yasiyoeleweka”.

Walijitenga na matokeo hayo.

Majaji wahoji sababu za makamishna kujiondoa dakika za mwisho

Chebukati alitangaza ushindi wa Dr. William Ruto wa chama cha United Democratic Alliance – UDA kwa kura milioni 7.18 (50.49%). Raila Odinga wa chama cha Orange Democratic Movement ODM, aliyepata kura milioni 6.94 (48.85%)

Matokeo hayo yamesababisha hisia kali za kisiasa nchini Kenya na kesi kufunguliwa mahakamani.

Katika kesi inayoendelea, Jaji Isaac Lenaola, alimuuliza wakili wa makamishna waliojitenga na matokeo hayo, kuieleza mahakama kama iwapo uamuzi wao wa kujitenga na matokeo haukuwa uamuzi wa mwisho baada ya kujua mshindi.

“Tuliona makamishna wakisoma matokeo ya uchaguzi wa urais kwenye televisheni. Nini kinafanya tusiamini kwamba uamuzi wao ulikuja baada ya zoezi?” Aliuliza Lenaona na mawakili wanatarajiwa kumjibu Ijumaa Septemba 2.

Muigai amesema hakuna Ushahidi katika madai ya Odinga

Wakili wa IEBC Githu Muigai, ameiambia mahakama kwamba mawakili wa Raila Odinga hawana Ushahidi wowote kwamba kulikuwa na udanganyifu katika uchaguzi huo.

Mawakili wa Odinga wameiambia mahakama kwamba idadi ya kura ambazo zilirekodiwa kwenye fomu ya matokeo katika vituo vya kupigia kura 34A, yalibadilishwa ili kuhakikisha kwamba Ruto anashinda uchaguzi huo.

Odinga pia amedai kwamba mfumo wa teknolojia wa IEBC ulidukuliwa na matokeo ya uchaguzi kubadilishwa. Pia, amedai kwamba kura zake zilipunguzwa katika kaunti za Bomet na Kiambu na kuongezewa Ruto.

Wakili Muigai amesema kwamba “kesi hii haina msingi wowote” na kwamba mawakili wa Odinga walizungumza “maneno yenye uzito mkubwa wakati wakiwasilisha madai yao dhidi ya tume ya uchaguzi lakini walipohitajika kutoa ushahidi walio nao, hawana lolote la msingi”.

Mawakili wa IEBC wamesisitiza kwamba tume ya uchaguzi iliandaa uchaguzi wa Agosti 9, 2022 kulingana na katiba, na kwamba Raila Odinga ana historia ya kukataa matokeo ya uchaguzi mkuu.

“IEBC haina shida yoyote. Wafula Chebukati hana tatizo lolote. Hakuna shida yoyote . Kuna shida na watu wanaoshiriki katika uchaguzi kukataa kushindwa au kushinda. Hiyo ndiyo shida,” Amesema Muigai.