Haya yanajiri huku chama kinachotawala cha Jubilee, kikizishutumu mahakama za nchi hiyo, kwamba zinakiuka sheria kwa kutoa maamuzi ambayo huenda yakachangia kuhairishwa kwa uchaguzi mkuu wa tarehe nane mwezi Agosti.
Kwa mujibu wa vyombo kadhaa vya habari nchini humo, likiiweno gazeti la Daily Nation, mkutano huo ulitarajiwa kufanyika katika hoteli ya Hilton, katikati mwa jiji la Nairobi.
Mwaliko wa mkutano huo uliotolewa na mwenyekiiti wa IEBC, Wafula Chebukati, ulifuatia uamuzi wa mahakama kuu ya Kenya wa kuitaka tume hiyo kusitisha uchapishaji wa karatasi za kupigia kura ya urais na kusema ilikosa kufuata kanuni na sheria kuhusu utoaji zabuni kwa kutoushirikisha umma ili kutoa maoni kuhusu uratibu wa kandarasi hiyo.
Kwenye uamuzi huo wa Ijumaa, majaji Joel Ngugi, John Mativo na George Odunga, aidha walikosoa tume hiyo kwa kukosa kuwashirikisha wadau wote kwenye zabuni hiyo ya Sh2.5 bilioni, iliyopewa kampuni ya Al-Ghurair kutoka Dubai.
Kesi hiyo, ilikuwa imewasilishwa na muungano wa Upinzani, NASA, ukilalamikia tume kwa kutozingatia sheria katika utoaji zabuni hiyo. IEBC imetangaza kwamba inakata rufaa, ili kutafuta ufafanuzi kuhusi mikakati ya jinsi ya kuhusisha umma katika utoaji wa zabuni hiyo.
Na kufuatia uamuzi huo wa mahakama, rais Uhuru Kenyatta, ambaye ndiye mgombea wa urais kwa chama cha Jubilee, aliikosoa mahakama kwa alichokiita kuingilia maandalizi ya uchaguzi kwa njia isiyofaa.
Akihutubu katika eneo la Kabartojo, Kaunti ya Baringo, siku ya Jumapili, rais huyo alisema kwamba amevumilia vya kutosha, na kuwa hataendelea kunyamaza huku idara hiyo "ikiweka vikwazo baada ya vikwazo kwenye mchakato wa maandalizi ya uchaguzi huo."
Matamshi ya Kenyatta yaliungwa mkonmo na naibu wake, William Ruto, pamoja na wanasiasa wengine wa mrengo wa Jubilee.
Hata hivyo, mgombea wa urais wa muungano wa upinzani (NASA), Raila Odinga, aliisifu mahakama kwa uamuzi wake na kusema kuwa hatua hiyo ni muhimu kuwahakikishia wapiga kura nchini humo kwamba uchaguzi utakuwa huru na wa haki.
JAJI MKUU JOHN MARAGA
Kufuatia matamshi ya rais Kenyatta kwamba mahakama zinaingilia kati masuala yasiyozihusu, jaji mkuu nchini Kenya, John Maraga, siku ya Jumapili alitoa taarifa ya kukanusha madai hayo akisema kuwa hawezi kuingilia kati maamuzi yanayotolewa na majaji na kwamba hajawahi kuitaka tume ya IEBC kusitisha uchapishaki wa karatasi za kura, kinyume na madai yaliyotolewa na naibu wa rais, William Ruto.
Wakati huo huo, tume ya IEBC iliwaalika raia kutuma nyaraka zenye maoni kuhusu utoaji wa zabuni ya karatasi za kupigia kura ya rais kufikia mwisho wa siku ya Jumanne, ili kutoa nafasi ya kikao kitakachohusisha umma, ambacho kitafanyika siku ya Jumatano, tarehe 12.
Mkutano wa Jumatatu kati ya IEBC na wadau wa uchaguzi mkuu wa Agosti, ulitarajiwa kutoa mwelekeo kwa suala ambalo wachambuzi wanasema huenda likawa na athari kubwa kwa mustakabali wa uchaguzi wa mwaka huu, na demokrasia kwa jumla, nchini humo.