Idadi ya wanainchi wa Afghanistan wasioweza kumudu chakula imeongezeka maradufu-Benki ya dunia.

Mamia ya wanaume wa Afghanistan wakusanyika kuomba msaada wa kibinadamu huko Qala-e-Naw, Afghanistan. Disemba 14, 2021. Picha ya AP.

Idadi ya watu nchini Afghanistan ambao hawawezi kumudu chakula na mahitaji mengine muhimu imeongezeka maradufu tangu wapiganaji wa Taliban wachukue uongozi wa nchi hiyo Agosti 2021, huku okosefu wa ajira ukiongezeka na mishahara kupungua, utafiti wa Benki ya dunia umeonyesha Jumanne.

Utafiti huo kuhusu ustawi wa wananchi wa Afghanistan, ambao ulifanyika kwa njia ya simu mnamo kipindi cha mwezi Oktoba mpaka Disemba 2021, uliona kuwa asilimia 70 ya waliohojiwa walisema familia zao haziwezi kugharamia mahitaji ya msingi ya chakula na yasiyo ya chakula, ikilinganishwa na asilimia 35 mwezi Mei 2021.

Karibu asilimia 50 ya familia ziliripoti pia kupungua kwa milo wanayotumia kila siku, ikilinganishwa na robo ya familia zilizohojiwa kati ya Julai na Agosti mwaka 2021.

Benki ya dunia ilihusisha hali ya umaskini na hali ya kiuchumi kwa ujumla badala ya hatua maalum zilizochukuliwa na utawala wa mpito, ikitaja hasa kupungua kwa nafasi za ajira katika sekta ya umma.

Viongozi wa Taliban hawajatambuliwa kimataifa miezi saba tangu wachukuwe udhibiti wa mji mkuu, Kabul, baada ya wanajeshi wa kimataifa wanaongozwa na Marekani kuondoka nchini Afghanistan, na hivyo kumaliza vita vya miaka 20.

Awali, Umoja wa mataifa ulionya kwamba zaidi ya nusu ya wananchi milioni 39 wa Afghanistan wanakabiliwa na njaa.