Idadi ya waliofariki dunia kutokana na tetemeko la ardhi la ukubwa wa 6.8 kwa vipimo vya rikta lililokumba maeneo ya Morocco Ijumaa usiku imeongezeka hadi zaidi ya watu 800, huku idadi ya waliojeruhiwa imepanda hadi 672, kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo.
Tetemeko hilo lilipiga Milima ya Atlas ya Morocco, kiasi cha kilomita 72 kutoka Marrakesh kivutio maarufu cha utalii.
Baadhi ya majengo yalitetemeka na kuporomoka mjini Marrakesh, na kuzilazimisha familia kukimbilia nje ambapo wengi wao walisema wangelala huko kwa usiku mzima wakiogopa kurudi kwenye nyumba zao zilizoharibiwa.
“Niliweza kuona majengo yakisogea. Hatupaswi kuwa na hisia kwa hali hii. Halafu nilitoka nje na kulikuwa na watu wengi," Abdelhak El Amrani mwenye umri wa miaka 33 mjini Marrakesh, aliiambia AFP.
Rais wa Marekani Joe Biden ameelezea masikitiko yake makubwa na kutoa salaam za rambi rambi kwa taifa na jamaa waliopoteza wapenzi wao katika tetemeko la ardhi lililotokea huko nchini Morocco.
Biden katika taarifa iliyotolewa na White House amesema amesikitishwa sana na kupotea kwa maisha na uharibifu uliosababishwa na tetemeko la ardhi Morocco. Mawazo na sala zetu ziko pamoja na wale wote walioathiriwa na hali hii mbaya. Utawala wangu unawasiliana na maafisa wa Morocco
Tunafanya kazi kwa haraka ili kuhakikisha raia wa Marekani walioko Morocco wako salama, na tuko tayari kutoa msaada wowote muhimu kwa watu wa Morocco. Marekani inasimama pamoja na Morocco na rafiki yangu Mfalme Mohammed VI katika kipindi hiki kigumu.”
Naye Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken pia ametuma salaam za rambi rambi kwa watu wa Morocco akiongeza kuwa Marekani iko pamoja nao katika wakati huu mgumu.