Idadi ya vifo yaongezeka Burkina Faso

Vikosi vya usalama kwenye mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou

Serikali ya Burkina Faso imesema Jumatano kwamba Idadi ya vifo kutokana shambulizi linaloshukiwa kufanywa na wanamgambo  kwenye kituo kimoja cha walinzi, kaskazini mwa taifa imeongezeka hadi 53. 

Shambulizi hilo linasemekana kuwa mbaya zaidi kwenye taifa hilo la Afrika Magharibi tangu mashambulizi ya kijihadi yalipoanza miaka 6 iliyopita. Msemaji wa serikali Qusseni Tamboura amesema kwamba jumla ya watu 53 wamethibitishwa kufa, wakiwemo walinzi 49 na raia wanne.

Wakati huo huo, shirika la msalaba mwekundu limesema kwamba idadi ya watu waliotoweka nchini humo imeongezeka mara nne kutoka 104 hadi 407 kati ya mwaka 2019 na 2020.Shirika hilo limeongeza kusema kwamba watu wametoweka nchini humo katika siku za nyuma kutokana na mafuriko pamoja na ongezeko la mashambulizi kutoka kwa wanamgambo.

Ingawa baadhi ya wanafamilia wanalaumu wanamgambo kutokana na kutoweka kwa watu wao, kuna wale wanaolaumu vikosi vya usalama. Ghasia zinazohusishwa na makundi ya al Qaida na Islamic State nchini Burkina Faso zimesababisha vifo vya maelfu ya watu wakati zaidi ya watu milioni 1 wakilazimika kutoroka makwao.