Idadi ya vifo vya kimbunga Freddy yafikia 190

Idadi ya vifo nchini Malawi kutokana na kimbunga Freddy imeongezeka hadi 190 Jumanne.

Hiyo ni baada ya dhoruba iliyovunja rekodi na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi kushambulia kwa mara ya pili barani Afrika chini ya wiki tatu.

Baada ya kujitengeneza Australia mapema Februari, kimbunga Freddy kilivuka bahari ya Hindi, na kuangukia kusini mashariki mwa Afrika mwishoni mwa Februari na kurejea wikendi kwa dhoruba ya pili.

Idara ya kukabiliana na majanga ya Malawi imesema idadi ya waliofariki imeongezeka kutoka 99 hadi 190, huku 584 wakijeruhiwa na 37 wakiripotiwa kutoweka.

Wafanyakazi wa kutoa misaada wanatarajia idadi hiyo kuongezeka.

Guilherme Botelho mratibu wa masuala ya dharura wa Madakrati wasio na mipaka amesema hali ni mbaya sana.

Aliongeza kusema kwamba kuna majeruhi wengi, na waliopoteza maisha huku pia idadi inaweza kuongezeka.