ICC kufungua ofisi Nairobi

Kenya imetia saini makubaliano na mahakama ya ICC kufungua ofisi zake mjini Nairobi.

Kenya imetia saini mkataba wa makubaliano kuiruhusu Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, kufungua ofisi yake mjini Nairobi ili kutekeleza shughuli zake kwa urahisi.

Zaidi ya mashahidi 400 wamekubali kufika mbele ya mahakama hiyo wakati wa kesi za watuhumiwa wa mauaji na ghasia za uchaguzi mkuu uliopita nchini humo.

Wakati wa sherehe hizo za utiaji saini mahakama ya kimataifa iliwakilishwa na msajili wake Bi Silvanor Aldi ambaye amekuwa nchini Kenya kwa uchunguzi wa machafuko yaliyotokea punde tu baada ya uchaguzi mkuu 2007.

Kwa upande wa serikali ya Kenya iliwakilishwa na mawaziri watatu George Saitoti, James Orengo na Amos Kingi.

Baaba ya makubaliano ya kutiwa saini msajili wa mahakama ya ICC, Bi Aldi, alisema ana matumaini kuwa serikali ya Kenya itaheshimu kikamilifu wajibu wake kuambatana na sheria iliyofikiwa mjini Rome kuhusu kazi na shughuli za ICC, pamoja na kutoa msaada kwa wafanyakazi wa mahakama hiyo katika utekelezaji wake.