Gavana wa eneo la Kherson Yaroslav Yanushevych, amesema kwamba amri ya watu kutotoka majumbani mwao kuanzia saa kumi na moja jioni hadi saa mbili asubuhi, inaendelea kutekelezwa kwa sababu za kiusalama.
Maafisa wamesema kwamba kampuni za mawasiliano ya simu zinafanya kazi kurejesha mawasiliano katika sehemu hiyo.
Wanajeshi wa Ukraine waliukomboa mji wa Kherson Ijumaa, baada ya wanajeshi wa Russia kuondoka mjini humo ambao ndio mji pekee waliokuwa wameudhibithi tangu walipoivamia Ukraine mwezi Februari.
Usafiri wa treni unatarajiwa kuanza tena wiki ijayo, kuelekea Kherson kutoka sehemu nyingine za nchi.
Wanajeshi wanaendelea kuondoa mabomu yaliyotegwa ardhini huku huduma muhimu zikirejea, japo maafisa wamesema kwamba hali katika mji huo ni ngumu.