Wataalam wanatabiri kuwa takriban watu milioni 80 watapiga kura kwa kutumia huduma ya posta mwaka huu, na ukusanyaji wa maoni unaonyesha kuwa idadi ya Wademokrat watakaopiga kura bila kwenda katika vituo vya kupiga kura ni mara mbili zaidi ya Warepublikan.
Trump ambaye yuko nyuma katika ukusanyaji wa maoni kitaifa, amerejea mara kadhaa kusema, bila ushahidi kamili, kwamba upigaji kura kwa njia ya posta una wizi na kughushi.
Majimbo mengi yamepanua wigo wa kupiga kura bila ya kwenda kituoni wakati huu wa janga la virusi vya corona ili kupunguza uwezekano wa kueneza ugonjwa weeny maambukizi ya juu na hatarishi kwa maisha ya watu.
Hasa hasa, Rais amekuwa mkosoaji wa majimbo yaliyoanza kutuma karatasi za kupiga kura kwa njia ya posta kwa wote waliosajiliwa kupiga kura, hata wale waliokuwa hawajaomba kufanya hivyo.
Wiki iliyopita mara mbili, Trump alikataa kuahidi kuwepo kukabidhiana madaraka kwa amani iwapo atashindwa uchaguzi, akieleza dukuduku lake juu ya uhalali wa kupiga kura kwa njia ya posta.
“Itabidi tusubiri tuone kitakachotokea. Mnajua kuwa nimekuwa nikilalamika kwa nguvu zote juu ya upigaji kura, na upigaji kura ni balaa,” amesema Trump wakati wa mkutano na waandishi wa habari Alhamisi.
Mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Demokratik Joe Biden amesema hashangazwi na kitendo cha Trump kupindisha maneno katika suala la kuhakikisha makabidhiano ya kidemokrasia ya madaraka kwa amani.
“Angalia, anasema vitu bila ya kutafakari kabisa,” Biden aliwaambia waandishi Jumatano jioni. “ Sijui niseme nini kuhusu hili. Lakini hili halinishangazi.”
Kiongozi wa waliowengi katika Baraza la Seneti la Marekani Mitch McConnell na viongozi wengine wa juu wa Warepublikan Alhamisi walisisitiza kuwa wanaunga mkono msingi wa kidemokrasia wa kukabidhiana madaraka kwa amani, bila ya kumkosoa rais moja kwa moja.