Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Rais wa Guinea Alpha Conde na viongozi kadhaa wa Afrika walikuwa wanatarajiwa kushiriki mazishi ya Deby, licha ya onyo la waasi waliowataka viongozi hao wasishiriki kwa sababu za kiusalama.
Deby aliiongoza Chad kwa zaidi ya miaka 30. Licha ya kukosolewa na makundi ya haki za binadamu kwa utawala wake wa kiimla, Deby alijiimarisha kama mshirika muhimu wa kijeshi wa madola ya magharibi, katika vita vya kimataifa dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu.
Kifo chake kilitangazwa na jeshi Jumanne, siku moja baada ya maafisa wa uchaguzi kusema kwamba alishinda muhula wa sita madarakani. Vyama vingi vya upinzani vilisusia uchaguzi.
Jana, gari ambalo lilikuwa na kipaza sauti lilizunguka mjini N’djamena likiwaambia wakazi kutokuwa na wasiwasi watakaposikia milio ya mizinga, Deby atapigiwa mizinga 21 ya kumpa heshma.