Hatimaye McCarthy amechaguliwa spika wa baraza la wawakilishi Marekani

Kevin McCarthy baada ya kuchaguliwa kuwa spika wa baraza la wawakilishi

Rais wa Marekani Joe Biden amesema kwamba yupo tayari kufanya kazi na warepublican, baada ya Mrepublican Kevin McCarthy kuchaguliwa kuwa spika wa baraza la Wawakilishi.

McCarthy alichaguliwa baada ya raundi 15 za upigazi kura ambao ulifanyika katika muda wa siku tano kutokana na wanachama wa Republican 20 wenye siasa za mrengo mkali wa kulia kupinga uteuzi wake.

Ushindi wake umepatikana baada ya kufikia makubaliano na wanasiasa hao.

Biden amesema atafanya kazi na Warepublican, na kwamba wapiga kura walionyesha dhahiri katika uchaguzi wa kati ya muhula kwamba Warepublican wanastahili kuwa tayari kushirikiana na utawala wa Biden.

Miongoni mwa mambo ambayo McCarthy amekubaliana na warepublican wenye siasa kali ni kuruhusu mwanachama kuitisha kura ya mapema ya kumchagua spika mwingine iwapo hawakubaliani na sera zake au namna anavyoongoza bunge.

Amewaahidi pia kuwaruhusu kusimamia shughuli za kamati muhimu na mapendekezo yao wanayoyaona muhimu kama kuweka kikomo cha mihula kwa wabunge na sheria kali za kudhibithi wahamiaji kwenye mpaka wa Marekani na Mexico.