Hamdok asimamisha magavana kazi, Sudan

Waziri mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdok

Waziri mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok amewasimamisha kazi makaimu  magavana wa majimbo walioteuliwa na kiongozi wa kijeshi baada ya mapinduzi yaliyofanyika mwishoni mwa Oktoba, kulingana na waraka ambao  shirika la habari la Reuters umeuona  Jumapili. 

Hamdock anasemekana kuweka watu wengine kwenye nafasi hizo, ikionekana kuwa hatua kuelekea kurejesha utawala wa kiraia baada ya mapinduzi ya kijeshi.

Kando na magavana, Hamdock pia anasemekana kufanya mabadiliko kwenye baraza la mawaziri lililowekwa na utawala wa kijeshi wakati baadhi ya walioondolewa wakisemekana kuwa watu wa karibu na kiongozi wa muda mrefu aliyeondolewa madarakani Omar al Bashir.

Hata hivyo Hamdock bado hajatangaza baraza jipya la mawaziri kama ilivyokubaliwa kwenye mkataba wa Novemba 21 kati yake na jeshi wakati akisemekana kukabiliwa na upinzani kutoka kwa baadhi ya vyama vya kisiasa, na waandamanaji.

Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya maandamano makali dhidi ya mapinduzi ya kijeshi pamoja na ukosoaji mkubwa kutoka jumuia ya kimataifa.