Kwa Waisraeli, inamaanisha kurejea kwa wanawake na watoto 50 kati ya jumla ya mateka 240. Kundi la kwanza la watu 13 waliachiliwa Ijumaa mchana - walipelekwa kwenye kivuko cha mpaka cha Rafah na kutoka huko walikwenda Israeli kwa helikopta.
Mateka hao walipelekwa katika hospitali tofauti nchini Israel ambako waliungana na familia zao. Afisa wa afya ya umma Dk. Hagai Levine anasema baadhi ya mateka ambao ni wazee walikuwa na magonjwa sugu kama vile kisukari. Watoto hawajaliona jua kwa takribani wiki saba.
“Hatujui, tunahitaji kujiandaa, tukiwa na imani kila kitu kitakwenda vizuri na kujiandaa kwa chochote kibaya kitakachotokea. Kwa hiyo, ndiyo maana huku Israeli tunatakiwa kuwa tayari kukidhi mahitaji yao, mtazamo kamili, baadhi yao mateka wamejeruhiwa vibaya sana, wamekatwa viungo vyao, mikono au miguu yao, majeraha ya risasi, hatujui jinsi gani na namna gani walivyotibiwa, na kama yalikuwa na kama walikuwa wamepata maambukizo,” Alisema Levine.
Kwa Wapalestina ina maana ya afueni kutoka katika vita vilivyodumu takribani wiki saba za mashambulizi ya anga ya Israel ambayo yameua zaidi ya Wapalestina 14,000, kulingana na wizara ya afya inayoshirikiana na Hamas.
Jason Lee, mkurugenzi wa Ukingo wa Magharibi wa Shirika la Save the Children, anasema watoto huko Gaza wameathiriwa kupita kiasi.
Sasa tuna hali ambapo mtoto mmoja huuawa kila baada ya dakika 10. Idadi ya raia ambao wamejeruhiwa inaongezeka pia. Zaidi ya raia 30,000 wamejeruhiwa, na tena, ikionyesha usawa wa vita hivi, karibu asilimia 70 - hiyo ni saba kati ya 10 - ni mwanamke au mtoto.
Sitisho la siku nne la vita litawapa wakaazi wa Gaza mapumziko na Israel imesema itaruhusu misaada mingi ya kibinadamu kuingia.
Siku ya Ijumaa, siku ya kwanza ya usitishaji mapigano, lori nne za mafuta na nne za mafuta ya kupikia, ziliingia Gaza.
Israel pia ilidondosha vipeperushi vya kuwaonya wakaazi wa kaskazini mwa Gaza ambao walikuwa wamekimbia mapigano kutorejea makwao, kwani mapigano yanatarajiwa kurejea mara baada ya kumalizika kwa sitisho la mapigano.