Hamas imekubali pendekezo la Marekani la kuanza mazungumzo juu ya kuwaachia huru mateka wa Israel wakiwemo wanajeshi na wanaume, siku 16 baada ya awamu ya kwanza ya makubaliano yanayolenga kumaliza vita vya Gaza chanzo kimoja cha Hamas kililiambia shirika la habari la Reuters leo Jumamosi.
Kundi hilo la wanamgambo wa kiislamu limeondoa madai kuwa Israel, kwanza ikubali makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano kabla ya kusaini mkataba wa makubaliano na kuruhusu mashauriano ili kufanikisha hilo katika kipindi cha wiki sita za awamu ya kwanza, chanzo hicho kiliiambia Reuters kwa masharti ya kutotajwa jina kwa sababu mazungumzo haya ni ya faragha.
Afisa mmoja wa Palestina ambaye yupo karibu na juhudi za kimataifa za mapatano ya amani alisema pendekezo hilo linaweza kupelekea mkataba wa makubaliano kama utakubaliwa na Israel na utamaliza miezi tisa ya vita kati ya Israel na Hamas huko Gaza.
Chanzo kimoja katika timu ya majadiliano ya Israel kikizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kilisema kwa sasa kuna fursa halisi ya kufanikisha makubaliano.
Hayo yalikuwa kinyume kabisa na matukio ya zamani katika vita vya miezi tisa huko Gaza, wakati Israel iliposema masharti yaliyowekwa na Hamas yalikuwa hayakubaliki.