Hali ya wasiwasi yaongezeka DRC kufuatia mvutano wa madaraka kati ya rais Tshisekedi na maafisa wa Kabila

Rais wa DRC Felix Tshisekedi.

Hali ya wasiwasi inaendelea kuongezea Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, kutokana na hali ya kutoelewana kati ya rais Felix Tshisekedi na watu wanaomuunga mkono rais wa zamani Joseph Kabila.

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Antonio Guteres, ameliambia baraza la usalama la umoja huo katika tipoti kwamba ana wasiwasi kuhusu mgogoro wa kisiasa katika muungano wa vyama vinayounda serikali Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Ameonya kwamba hali hiyo inaweza kuvuruga hali ya kisiasa nchini humo na kuharibu mafanikio ambayo yamepatikana tangu mwaka 2018 ikiwemo kukabidhiana madaraka kwa njia ya amani na kutatua changamoto za kiusalama katika sehemu kubwa ya nchi hiyo.

Kuna video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha kiongozi wa kikosi cha ulinzi wa rais Felix Tshisekedi anawaamuru walinzi wake kutopanga mapinduzi dhidi ya serikali.

Maafisa wa ngazi ya juu katika serikali ya DRC waliteuliwa na Joseph Kabila aliyeondoka madarakani mwaka 2019 baada ya kutawala nchi hiyo kwa miaka 18.

Ubadilishanaji wa madaraka

Hatua ya Kabila kumpokeza Tshisekedi madaraka kwa njia ya amani ilikuwa ya kwanza kuwahi kutokea tangu nchi hiyo ilipopata uhuru kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960.

Mipango ya Tshisekedi ya kuleta mabadiliko nchini humo imekwamba kutokana na vizingiti vya kutakiwa kufanya kazi na muungano wa vyama vya kisiasa vinavyoongozwa na watu waliokaribu san ana rais mstaafu Joseph Kabila.

Muungano wa vyama hivyo una idadi kubwa ya wabunge bungeni.

Inatarajiwa kwamba rais Tshisekedi atatangaza maamuzi yake hivi karibuni baada ya kufanya mashauriano.

Tangazo lake linasubiriwa kwa wasiwasi sana nchini humo na kuzua uvumi mjini Kinshasa.

Mvutano waonekana hadharani

Viongozi katika chama cha rais Tshisekedi cha UDPS, wamekuwa wakimhimiza kujiondoa kwenye mkataba na Kabila wa Januari 2019, ambao yaliyomo hayajawekwa wazi kwa uma.

Hali ya mvutano ilionekana wazi mwezi July baada ya Tshisekedi kuteua majaji watatu wapya katika mahakama kuu, baraza la kikatiba na kupelekea malalamiko katika chama cha FCC.

Viongozi wa FCC walisusia sherehe ya kutawazwa kwa majaji hao iliyofanyika Oktoba 21.

Katika hotuba kwa taifa siku mbili baadaye, Tshisekedi alikiri kuwepo hali ya kutoelewana kuhusu usalama wa taifa, usimamizi wa mali za taifa, uhuru wa mahakama na usimamizi wa uchaguzi mkuu.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC