Mapigano yamekuwa makali zaidi kati ya waasi wa M23 ambao serikali ya Kinshasa inadai kuwa ni jeshi la Rwanda ambalo limejipa jina la M23 , ndiyo wako kwenye uwanja wa mapigano kupambana na wanajeshi wakiwemo jeshi la Congo FARDC.
Wapiganaji Wazalendo, SADC na wengine ambao wako nchini DRC kuliunga mkono jeshi la serikali ambalo linapambana na kile kinachoitwa uvamizi.
Jumamosi kikosi cha Umoja wa Mataifa MONUSCO kimepoteza wanajeshi wake wawili na wengine wanne kujeruhiwa baada ya bomu moja kutoka upande wa waasi wa M23 kushambulia gari lao la kijeshi eneo la Kasengezi pembeni mwa kambi ya wakimbizi ya Mugunga katika barabara ya kuelekea Sake magharibi mwa mji wa Goma.
Hadi sasa MONUSCO haijasema lolote ila serikali ya DRC imeiomba Umoja wa Mataifa kuwachukulia hatua waasi hao ambao waungwa mkono kijeshi na serikali ya Rwanda.
Vita mashariki mwa Congo vimeleta hasara kubwa kwa wananchi wa kawaida ,hasa wanawake na watoto na kuwalazimisha vijana kujiunga katika makundi mbali mbali ya waasi ikiwemo lile la wazalendo na pia la M23 kwa ukosefu wa ajira na kutokuwa na usalama wa kutosha.
Mumbere Syavulisembo maarufu Poutine amekuwa miongoni mwa watu wanao unga mkono hatua ya vijana kujiunga na wazalendo kulipigania taifa lao, lakini vijana hao wakiwa hawana mafunzo ya kijeshi ila wakifahamu kutumia silaha na huwa ndio wamekuwa wakionekana mstari wa mbele wa mapigano.
Wafanya kazi wengi wa kimataifa wameanza kuondoka katika Mji wa Goma kuona kana kwamba mapigano yanaendelea na serikali ya Kinshasa ikiendelea kukataa kufanya mazungumzo na waasi .
Marekani iliomba Congo kuzungumza na M23 kama njia moja ya suluhisho lakini Rais wa DRC Felix Tshisekedi amekataa akisema haiwezekani ila yuko tayari kuzungumza na Rwanda.
Siku ya Alhamisi Gavana wa Kivu Kaskazini Meja Jenerali Peter Cirimwami alifariki dunia baada ya kupigwa risasi kwenye uwanja wa mapambano kwenye bonde la mji wa Sake ambako kuna kambi kubwa ya UN na SADC, serikali iliwaomba wanajeshi na wapiganaji Wazalendo kulipiza kisasi kwa kuyakomboa maeneo yote yanayodhibitiwa na M23.
Naye naibu Gavana wa Jenerali Ekuka Lipopo amesema hawataondoka Goma, ila watapigana na M23 iwapo itajaribu kuingia Goma na hii itaingia katika historia ya Congo na watakao baki wataandika hadithi amesema Lipopo.
Kwa sasa bado hali inaendelea kuwa ya wasiwasi mkubwa kutokana na wingi wa silaha mjini Goma.