Mapigano yamepamba moto katika taifa hilo la Afrika Kaskazini tangu katikati mwa mwezi Aprili, wakati mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Dagalo, ambaye anaongoza kikosi cha dharura cha (RSF), waliposhambuliana.
Makubaliano kadhaa ya kusitisha mapigano yalifikiwa na kukiukwa tangu mzozo ulipozuka, na Marekani iliwawekea vikwazo majenerali hao hasimu baada ya juhudi za mwisho za kusitisha mapigano kukwama mwishoni mwa mwezi Mei.
Mashambulizi ya anga na mizinga ambayo yamekuwa yakiutikisha mji wa Khartoum kila siku yamepungua angalau kwa muda, na kuruhusu raia waliokwama katika mapigano kutoka nje na kununua bidhaa zinazohitajika sana.
Katika soko moja la Khartoum, watu walionekana wakihangaika kutafuta matunda na bidhaa nyingine msingi.