Serikali ya Ufaransa imetangaza mipango ya kuongeza kwa miezi mingine miwili hali ya dharura ambayo iliwekwa baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Novemba mjini Paris ili kuendana na matukio mawili makubwa ya michezo ya kimataifa, huku watalaamu wakionya kuhusu vitisho vipya vinavyoikabilia Ulaya.
Waziri Mkuu Manuel Valls amesema serikali inataka kuongeza muda wa hali ya dharura ambayo awali ilitarajiwa kumalizika May 26 ili kutoa dhamana ya usalama kwa mashindano ya kandanda ya Euro 2016 na mbio za baiskeli za Tour de France.
Euro 2016 inatarajiwa kuanza Juni 10 kwa kipindi cha mwezi mmoja, wakati Tour de France inaanzza Julai 2 hadi 24.
Ufaransa ni nchi pekee ya Ulaya kutangaza hali ya dharura kwasababu ya ugaidi, kuchukua hatua baada ya mashambulizi ya Novemba na mashambulizi ya mabomu kuzunguka mji mkuu ambayo yaliua watu 130.