Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres anawahimiza wafadhili kuheshimu ahadi walizotowa katika mapambano ya Ebola. Guterresh alieleza hayo wakati alipotembelea Congo kuonesha uungaji mkono wake katika mapambano dhidi ya mlipuko wa ugonjwa huo.
Aliwaambia waandishi wa habari mjini Kinshasa kwamba Umoja wa Mataifa umepokea asilimia 15 pekee ya kile kinachohitajika katika mapambano ya mlipuko wa Ebola kwa mwaka huu. Alieleza hayo kabla ya kukutana na Rais wa Congo, Felix Tshisekedi.
Na katika tukio jingine siku ya Jumatatu waziri wa zamani wa afya wa Congo, Oly Ilunga, alihojiwa na polisi juu ya namna alivyosimamia fedha za kupambana na mlipuko wa Ebola. Ilunga alijiuzulu wadhifa huo mwezi Julai baada ya kusimamia juhudi za serikali kupambana na mlipuko wa Ebola kwa takribani mwaka mmoja.
Mawakili wa Ilunga walisema alikuwa akihojiwa kuhusu malipo ambayo ofisi yake ililipa kwa wakuu wa kijiji ili kusaidia kusambaza taarifa kuhusu ugonjwa wa Ebola pamoja na bahasha zilizogawiwa kwa wafanyakazi wake. Mawakili hao walikanusha Ilunga hakuhusika na suala lolote kinyume cha sheria.