Guterres aonya kuhusu ongezeko la silaha za nyuklia ulimwenguni

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (kushoto) kwenye ufunguzi wa kikao cha NPT mjini New York Jumatatu

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Jumatatu wakati wa ufunguzi wa kongamano la kupinga utengenezaji wa silaha za nyuklia mjini New York  amesema kwamba kuna hatari ya kuongezeka kwa utengenezaji wa silaha hizo.

Hali hiyo amesema ni kutokana na udhaifu kwenye mikakati iliyowekwa ya kuzuia. Guterres amesema kwamba ulimwengu wa sasa uko umbali wa hatua moja tu ya sintofahamu au kutokuwa na udhibiti wa kutosha , kujielekeza kwenye maangamizi ya nyuklia.

Wakati wa ufunguzi wa kikao hicho maarufu kama Nuclear Non proliferation Treaty, NPT, Guterres ameonya kwamba kuna mizozo ya kinyuklia inayotokota kuanzia mashariki ya kati hadi kwenye Peninsula ya Korea pamoja na kutokana na uvamizi wa Russia wa Ukraine.

Ameongeza kusema kwamba kuna karibu silaha 13,000 ziliozopo kote ulimwenguni, na kwamba watu huenda wamesahau walichojifunza kutokana na vita vya pili vya dunia wakati mataifa yakitafuta vigezo vya kuendelea kujiwekea silaha, huku yakitumia mabilioni ya fedha kwa ajili ya silaha zinazoweza kuangamiza dunia.

Kiongozi huyo amesema kwamba atasafiri Japan ili kuhudhuria maadhimisho ya tarehe 6 Agosti mjini Hiroshima, ambapo Marekani iliangusha bomu la kwanza la Atomic miaka 77 iliyopita kama juhudi ya kumaliza vita vya pili vya dunia.