Ghasia zaripotiwa Zanzibar, upigaji kura waanza

Rais wa Tanzania John Magufuli

Wanasiasa wa upinzani wanasema kwamba watu 10 waliuawa huku kukiwa na wasiwasi mkubwa iwapo uchaguzi wa Jumatano utakuwa huru na haki.

Hali ya wasiwasi inaendelea kutanda visiwani Zanzibar baada ya ghasia kutokea Jumanne, saa chache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu.

Wanasiasa wa upinzani wanasema kwamba watu 10 waliuawa huku kukiwa na wasiwasi mkubwa iwapo uchaguzi wa Jumatano utakuwa huru na haki.

Rais wa Tanzania John Magufuli amewataka wapiga kura kupiga kura kwa amani naye mpinzani wake mkuu katika kuwania urais, Tundu Lissu akihitimisha kampeni zake Jumanne amewasihi wafuasi wake kupiga kura kwa utulivu.

Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha upinzani ACT Wazalendo, Seif Sharif Hamad alikamatwa Jumanne na kuachiliwa baadaye.

Amesema kwamba watu 10 wameuawa katika ghasia kwenye kisiwa hicho, kabla ya upigaji kura.

"Wamekuwa wakitumia risasi za moto dhidi ya watu. Hesabu tuliyo nayo hadi sasa ni vifo vya watu 10 Zanzibar, 9 Pemba na 1 Unguja.” Amesema Seif Hamad,

Alizuiliwa kwa muda wa saa kadhaa baada ya kujaribu kupiga kura Jumanne, ambayo ni siku maalum iliyotengwa kwa maafisa wa usalama kupiga kura.

Ameuelezea uchaguzi huo kuwa “kejeli”, akisema kwamba “unawezaje kuandaa uchaguzi katika mazingira ya kurusha gesi ya kutoa machozi na risasi za moto kila mahali? Huu sio uchaguzu huru na haki, ni kejeli tu.”

"Kila chama cha siasa kinastahili kuwa na wakala kulinda maslahi ya chama. Mawakala wetu wamefukuzwa kutoka kwenye vituo vya kupigia kura. Kwa nini? Kwa sababu maafisa wa uchaguzi ambao wanastahili kutoa karatasi moja kwa kila mpiga kura wanatoa karatasi mbili au tatu kwa mpiga kura mmoja.”

Kwenye visiwa vya Zanzibar, ambavyo huchagua rais wa Tanzania bara, pamoja na kiongozi wao wakiwemo wabunge na wajumbe wa baraza la wawakilishi, vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kwamba maafisa wa usalama wametumia gesi ya kutoa machozi na risasi za moto, pamoja na kuwapiga raia.

Inspekta Mkuu wa jeshi la polisi Tanzania Simon Sirro amewaambia waandishi wa habari jijini Dar-es-salaam kwamba watu 42 wamekamatwa Pemba, lakini amekanusha ripoti za kutokea vifo.

Ghasia za uchaguzi visiwani Zanzibar zinajiri wakati kuna wasiwasi kuhusu uchaguzi wa Tanzania.

Miaka mitano ya utawala wa rais Magufuli umeshuhudia msako dhidi ya wanasiasa wa upinzani na ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza.

Katika siku ya mwisho ya kampeni, Magufuli amewasihi watu kupiga kura na kurudi nyumbani ili watoe mazingira mazuri kwa tume ya uchaguzi kufanya kazi yake. Ametaka watu wote kudumisha amani.

Tundu Lissu, ambaye ameongeza nguvu kwa upinzani baada ya kurejea Tanzania kutoka Ulaya alikokuwa anatibiwa kwa muda wa miaka mitatu baada ya kunusurikay kifo alipopigwa risasi mara 16, ameandaa mikutano mikubwa wa kampeni kuelekea uchaguzi wa Jumatano.

"Nimeshuhudia katika mikutano ya kampeni kwamba Tanzania ipo tayari kwa mabadiliko na naamini kwamba watajitokeza kwa wingi kupiga kura.” Amesema Tundu Lisu.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC