Ghasia zapamba moto Kenya

Wafuasi wa upinzani wakikusanya mawe na matairi wakati wakipambana na maafisa wa polisi katika eneo la Mathare, jijini Nairobi tarehe 27 Machi, 2023. Picha na Luis Tato / AFP.

Mwanamme mmoja ambaye jina lake halija julikana aliuawa kwa kupigwa risasi siku ya Jumatatu wakati wa maandamano katika mji wa Kisumu, uliopo magharibi mwa Kenya, George Rae Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga iliyoko Kisumu aliliambia shirika la habari la AFP.

Hiki ni kifo cha pili kuripotiwa tangu maandamano kuanza Jumatatu iliyopita ambapo mwanafunzi wa chuo kikuu aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi.

Tangu maandamano hayo ya kuipinga serikali yaanze wiki iliyopita ghasia zimekuwa zikiongezeka huku polisi wakitumia mabomu ya kutoa machozi kwa msafara wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga na wafuasi wake, wakati waporaji wakiendelea kufanya fujo.

Mwanasiasa huyo mkongwe ameitisha maandamano kila Jumatatu na Alhamisi akimshutumu Rais William Ruto kwa wizi wa kura wakati wa uchaguzi wa mwaka jana na kushindwa kudhibiti kupanda kwa gharama ya maisha.

Waandamanaji hao walikaidi onyo la Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome kwamba maandamano ya Nairobi na Kisumu ambako ni ngome ya Odinga ni kinyume cha sheria.

Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi ili kuutawanya umati wa watu mjini Nairobi pamoja na Kisumu na kuyaathiri magari yaliyokuwa yamewabeba waandishi wa habari waliokuwepo katika mji mkuu huo.

Maafisa pia walitumia gesi ya kutoa machozi na maji ya kuwasha wakati msafara wa Odinga ulipokuwa ukipita katika eneo lenye msongamano jijini Nairobi, na kuwafanya watu kukimbia wakitafuta pa kujihifadhi.

Wakiwa wameshika mapanga na marungu, makundi ya waporaji yamenaswa kwenye kamera wakiwaonyeshwa wakibeba wanyama kama kondoo na kuwapakia kwenye magari yao. Mpaka sasa maafisa wa polisi nchini Kenya hawajatoa taarifa ya kina.

Muda mfupi baadaye, vyombo vya habari vya Kenya, pia vimeripoti habari za uvamizi katika kampuni ya kiongozi huyo wa upinzani Raila Odinga, kampuni iliyosemekama kutengeneza mitungi ya gesi ijulikanayo kama East Africa Specter International iliyoko katika eneo la viwanda, lililoko nje kidogo mwa jiji la Nairobi.

Baadhi ya taarifa za habari hii zinatoka shirika la habari la AFP.