FIFA yamsimamisha kwa muda rais wa shirikisho la soka la Uhispania

Mchezaji Jennifer Hermoso na rais wa shirikisho la soka la Uhispania Luis Rubiales wakisherekea ushindi wa kombe la dunia la wanawake, kwenye uwanja wa Sydney Australia, Agosti 20, 2023

Kamati ya nidhamu ya shirikisho la soka duniani (FIFA) imemsimamisha kwa muda mkuu wa shirikisho la soka la Uhispania Luis Rubiales kwa siku 90, FIFA imesema leo Jumamosi.

Kitendo cha Rubiales kushika kichwa cha mchezaji Jenni Hermoso na kumbusu mdomoni baada ya ushindi wa Uhispania kwenye kombe la dunia la wanawake, kilizua gumzo.

Rubiales alitarajiwa kutangaza kujiuzulu siku ya Ijumaa lakini badala yake akasema hatajiuzulu, na shirikisho la soka la Uhispania (RFEF) lilitishia kuchukua hatua za kisheria kumtetea baada ya Hermoso kusema kuwa Rubiales alimbusu bila ridhaa yake.

“Mwenyekiti wa kamati ya nidhamu ya FIFA, leo ameamua kumsimamisha kwa muda bwana Luis Rubiales kwenye shughuli zote zinazohusiana na soka kwenye ngazi ya taifa na kimataifa,” FIFA ilisema katika taarifa.

Kamati ya nidhamu imemuamuru Rubiales na maafisa na wafanyakazi wa RFEF kujizuia kuwasiliana au kujaribu kuwasiliana na Hermoso au wale walio karibu naye.

Timu ya taifa ya Uhispania ambayo ilishinda kombe la dunia pamoja na wachezaji wengine kadhaa walisema hawatacheza mechi za kimataifa wakati Rubiales ataendelea kuwa mkuu wa shirikisho la soka.