Viongozi wa Umoja wa Ulaya Alhamisi waliitaka China kurekebisha ukosefu wa uwiano wa kibiashara wa nchi hiyo na Ulaya na kuishinikiza Russia, kumaliza vita yake nchini Ukraine.
Katika mazungumzo ya kwanza ya ana kwa ana katika muda wa zaidi ya miaka minne kati ya wakuu wa China na Umoja wa Ulaya, rais wa China, Xi Jinping, na waziri mkuu Li Qiang, walikutana mjini Beijing, na Charles Michel, ambaye ni rais wa baraza la Ulaya, na Ursula von der Leyen, rais wa tume ya Ulaya.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Von der Leyen alizungumza na rais Xi kuhusu uhusiano wa karibu wa Beijing na Kremlin, amesema China inaweza kufanya zaidi katika kukomesha uchokozi wa Russia, dhidi ya Ukraine.
Kama mshirika mkuu wa biashara wa Russia, China imemsaidia rais wa Russia, Vladimir Putin kukwepa vikwazo vya mataifa ya magharibi vilivyo lenga kuuadhibu uchumi wa taifa lake.