Umoja wa Ulaya umeishutumu China, Jumapili kwa kuchukua hatua hatari dhidi ya Ufilipino, huku Beijing na Manila zikilaumiana kwa kuhujumu kimakusudi meli zao za walinzi wa pwani.
Mgongano huo ni wa karibuni zaidi katika mfululizo wa matukio kama hayo katika wiki za kadha zilizopita katika bahari ya South China, ambapo Beijing inadai kumiliki eneo lote muhimu la kiuchumi la bahari licha ya madai ya ushindani kutoka kwa nchi nyingine na uamuzi wa mahakama ya kimataifa kwamba madai yake hayana msingi wa kisheria.
“EU inalaani kitendo cha hatari cha meli za walinzi wa pwani wa China, dhidi ya operesheni halali ya baharini ya Ufilipino katika eneo la Sabina Shoa,” Nabila Massrali, msemaji wa mwanadiplomasia mkuu wa EU, Josep Borrell, amesema katika taarifa.
Msemaji wa kikosi cha China, Jumamosi alisema kwamba tukio hilo lilitokea nje ya eneo lenye mgogoro la Sabin Shoal, ambalo ni kitovu cha mgogoro wa bahari hiyo.