EU kuongeza ushuru kwa magari ya umeme ya China

Tume ya Ulaya, Jumatano imesema inapanga kuongeza ushuru wa hadi asilimia 38 kwa magari ya umeme ya China, yanayoagizwa kuanzia Julai, hatua ambayo inaongeza mzozo wa kibiashara ambao Brussels inaona kama sehemu ya juhudi za kulinda viwanda vya mataifa ya EU.

Hatua hiyo ambayo maafisa wa Beijing, wameshutumu kuwa kama kinga, inafanyika ikiwa ni chini ya mwezi mmoja baada ya Washington, kuongeza ushuru kwa magari ya umeme ya China hadi kufikia asilimia 100.

Chombo cha utawala cha EU, kimesema uamuzi wake wa karibu mara nne kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 10 umefikiwa baada ya uchunguzi, mwingine ukiendelea ikiwa wazalishaji wa teknolojia safi ya China wanatupa bidhaa zinazofadhiliwa na serikali kwenye masoko ya EU, na kuwapa watengenezaji magari wa China faida isiyo ya haki.