Umoja wa Ulaya Jumapili umetoa pendekezo la kuimarisha ushirikiano na Tunisia ambalo linajumuisha msaada wa kifedha wa muda mrefu ambao unaweza kufikia kiwango cha euro milioni 900 na msaada wa ziada wa mara moja wa euro milioni 150 kwa taifa hilo.
Rais wa tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, akiwa ziarani Tunisia, amesema kuwa amependekeza mpango huo wenye vipengele vitano kwa Rais Kais Saied, ikiwemo msaada wa kifedha ili kupambana na uhamiaji haramu.
Ameelezea matarajio yake kuwa makubaliano kati ya Umoja wa Ulaya na Tunisia yatasainiwa kwenye mkutano ujao wa Umoja wa Ulaya ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.
“Ni kwa maslahi yetu ya pamoja kuimarisha uhusiano wetu na kuwekeza katika uthabiti na maendeleo, ni kwa sababu hiyo tupo hapa,” alisema von der Leyen.