Umoja wa Ulaya umeelezea wasiwasi kuhusu vurugu za baada ya uchaguzi nchini Chad, siku nne baada ya ushindi katika uchaguzi wa rais wa kiongozi wa kijeshi Jenerali Mahamat Idriss Deby Itno.
Baada ya matokeo kutangazwa siku ya Alhamisi, wanajeshi walifyatua risasi hewani katika mji mkuu wa Chad, N'Djamena, katika sherehe na kuwazuia waandamanaji, waandishi wa habari wa AFP waliripoti.
Vyombo vya habari vya Chad vimeripoti kuwa kuna vifo kadhaa vilivyotokea pamoja na majeruhi kutokana na “shangwe za furaha”, lakini serikali ilikataa kutoa idadi hiyo na kuzizuia hospitali kufanya hivyo, ikieleza ni kuheshimu usiri katika matibabu.
Wafuasi wa Deby walifyatua risasi hewani katika sherehe karibu na makazi ya rais. Takriban vijana wawili walijeruhiwa kwa kupigwa risasi, kulingana na mwandishi wa habari wa AFP.