Katika mkutano wa NATO uliofanyika mwishoni mwa mwezi Juni mjini Madrid, Erdogan aliziomba nchi hizo mbili kutekeleza wajibu wao katika mapambano dhidi ya ugaidi na akazishtumu kwa kutoa hifadhi salama kwa wanamgambo wa Kikurdi wasiotambuliwa na sheria za Uturuki.
Akizungumza Jumatatu, siku moja kabla ya mkutano wa pande tatu na Russia na Iran, Erdogan amewambia waandishi wa habari “ Nataka kusisitiza tena kwamba tutasimamisha mchakato ikiwa nchi hizi hazitachukua hatua zinazohitajika kutimiza masharti yetu”.
“Haswa tumeona kwamba Sweden haina taswira nzuri kuhusu suala hili,” ameongeza kiongozi huyo wa Uturuki.
Mapema mwezi huu, NATO ilianza utaritibu wa kuziruhusu Sweden na Finland kujiunga na muungano huo baada ya kufikia makubaliano na Uturuki, ambayo ilikuwa imeyazuia mataifa hayo ya Ulaya kaskazini kujiunga na NATO.
Erdogan alizishtumu nchi hizo mbili kuwa kimbilio la wanamgambo wa Kikurdi, hasa akiangazia chama kilichoharamishwa cha wafanyakazi wa Kurdistan (PKK) ambacho alitaka kukiangamiza, kwa tuhuma za kuimarisha “ugaidi”.