Khashoggi: Uturuki yaendelea kuishutumu vikali Saudia

Rais wa Uturuki Recep Yayip Erdogan

Rais wa Uturuki Recep Tayip Erdogan ameendelea kutoa shinikizo kali kwa Saudi Arabia kufuatia kuuawa kwa  mwandishi wa habari Jaml Khashoggi, katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul mwezi jana katika mazingizra yaliyozua utata.

Jumanne, gazeti linalomilikiwa na serikali ya Uturuki liitwalo Sabah, lilichapisha picha za X-Ray na kudai kwamba zilionyesha vifaa vilivyotumika kwa mauaji ya Khashoggi, vikiwa ndani ya sanduku lililobebwa na watu waliokuwa wametoka Saudi Arabia.

Ripoti iliyoandikwa kwenye gazeti hilo, imetajwa na wachambuzi kama hatua ya hivi karibuni kabisa ya kampeni kabambe iliyopangwa na Ankara dhidi ya Riyadh, ikikusudiwa kuwafichua waliohusika kwa kifo cha mwandishi huyo, aliyekuwa mosoaji mkubwa wa utawala wa ufalme wa Saudia.

Wiki jana, Rais Erdogan alisema kwamba sauti zilizorekodiawa wakati Khashoggi aliuawa, zimetumwa kwa Marekani, Saudi Arabia, na nchi zingize zenye nguvu za bara ulaya.

Tangu kuuawa kwa Khashoggi tarehe mbili mwezi uliopita, Ankara, kwa taratibu, imekuwa ikitoa ripoti kwa vyombo vya habari juu ya yale inayosema yalitukia kwenye ubalozi huo mdogo.

Wachambuzi wanasema utaratibu huo wa kutoa habari kila baada ya muda fulani, umedumaza matuamaini ya Riyadh kwamba gumzo kuhusu sakata hiyo, litafifia.

Mwana wa mfalme wa Saudia, Mohamed Bin Salman, ambaye anashutumiwa kuhusika kwa sakata hiyo, ameendelea kukanusha kwamba ufalme ulihusika kwa vyovyote katika mauaji hayo.