Mamia ya maelfu ya waumini wamekusanyika Equador Jumatatu ili kupata nafasi ya kuhudhuria misa ikiongozwa na Papa Francis aliyeanza ziara ya siku tatu nchini humo kwa misa ya halaiki kwenye mji wa bandari wa Guayaquil ulioko kusini magharibi.
Kiongozi huyo wa kanisa katoliki mwenye umri wa miaka 78 wa kundi la Jesuit aliwasili jumapili katika mji mkuu Quito ukiwa mkondo wa kwanza wa ziara yake. Wakuu wa serikali na viongozi wa kanisa walijitokeza kumlaki pamoja na watoto waliokuwa wamevalia mavazi yenye rangi rangi huku watu wazima wakipeperusha vibendera vya papa wakiwa kando ya zulia jekundu.
Anatarajiwa kurejea mji mkuu Jumanne kwa ibada nyingine katika bustani ya Bicentennial kabla ya kuelekea Bolivia na Paraguay. Papa Francis hatatembelea nchi yake asili ya Argentina lakini anapanga kufanya ziara mwaka ujao.