Seneta m-democrat Elizabeth Warren wa Marekani ameunda kamati ya uchunguzi kwa ajili ya kuwania urais mwaka 2020. Seneta huyo wa Massachusetts siku ya Jumatatu alikuwa mtu wa kwanza katika kile kilichobashiriwa kutangaza azma yake ya urais ifikapo 2019.
Warren mwenye miaka 69 alizungumza kwenye video iliyotumwa kwa wafuasi wake akisema “hata kama tuna tofauti zetu, wengi wetu tunataka kitu hicho hicho. Kuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa bidii na kuwahudumia watu tunaowapenda. Hicho ndicho ninachopigania na ndio maana leo ninazindua kamati ya uchunguzi kwa ajili ya kuwania urais”.
Kamati hiyo inamuwezesha kuchangisha fedha na kujaza nafasi za wafanyakazi kabla ya kuanza rasmi kampeni zake za urais baadae mwaka huu wa 2019.