Wamisri waandamana tena kwenye uwanja wa Tahriri

  • Mkamiti Kibayasi

Waandamanaji nchini Misri wakiwa katika uwanja wa Tahriri, Ijumaa, November 18, 2011

Wakazi wa Misri leo wamekusanyika tena kufanya maandamano wakidai utawala wa jeshi kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia

Maelfu ya Wa-misri wanaandamana kwenye uwanja wa Tahrir mjini Cairo, wakikasirishwa na kile wanachokisema ni jaribio linalofanywa na jeshi nchini humo kuimarisha utawala wake.

Maandamano ya Ijumaa yaliitishwa na kundi la Muslim Brotherhood, kundi pekee lililojipanga kisiasa nchini humo kwa wakati huu, katika kujibu pendekezo la serikali kuliruhusu jeshi kua na uwamuzi wa mwisho kuhusiana na sera kuu.

Waandamanaji na vyama vingine vya kisiasa pia wanadai ratiba inayoeleweka kwa jeshi kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia.

Wa-Misri wanatarajiwa kwenda kwenye vituo vya kupigia kura baadae mwezi huu kuanza utaratibu wa kuchagua bunge jipya. Upigaji kura huo ni wa kwanza tangu kutokea upinzani wa raia ulomuondoa madarakani mtawala wa muda mrefu wa Misri, Hosni Mubarak.