ECOWAS yakataa pendekezo la utawala wa kijeshi Niger kwamba uchaguzi ufanyike ndani ya miaka 3

PICHA YA MAKTABA: Mkutano wa kamati ya wakuu wa kijeshi wa jumuiya ya ECOWAS

Jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi, ECOWAS, imekataa pendekezo la utawala wa kijeshi wa Niger la kutaka uchaguzi ufanyike ndani ya miaka mitatu, na kuzidisha mzozo wa kisiasa ambao unaweza kusababisha uingiliaji wa kijeshi, kama hakuna makubaliano yatakayofikiwa kufuatia mapinduzi ya Julai.

ECOWAS na wasuluhishi wengine wenye nguvu, wamekuwa wakitafuta suluhu ya kidiplomasia, kwa mapinduzi hayo ya Julai 26 nchini Niger, ambayo ni ya saba katika ukanda wa Afrika Magharibi na Kati, katika kipindi cha miaka mitatu.

Lakini baada ya juhudi kadhaa kushindikana, jumuiya hiyo - ambayo imechukua msimamo mkali zaidi kuhusu Niger kuliko majirani zake wanaoongozwa kijeshi - ilianzisha kikosi cha kikanda ambacho wakuu wa kijeshi wamesema kiko tayari kupelekwa nchini humo iwapo mazungumzo hayatafanikiwa.

Hivi karibuni, ECOWAS ilisisitiza, kwa mara nyingine, tishio lake la kuingilia kati kijeshi, siku moja kabla ya utawala wa kijeshi hatimaye kukubali kukutana na ujumbe wa ECOWAS katika mji mkuu Niamey, na kupelekea nia mpya ya kushirikiana.

Katika hotuba yake kwa taifa kwa njia ya televisheni Jumamosi jioni, kiongozi wa utawala wa kijeshi Jenerali Abdourahamane Tiani, alisema viongozi wa mapinduzi bado wako tayari kwa mazungumzo.

Kamishna wa ECOWAS Abdel-Fatau Musah aliiambia Reuters siku ya Jumatatu kwamba msimamo wa jumuiya hiyo bado uko wazi, kwamba ni lazima utawala wa kikatiba urejeshwe mara moja, na kiongozi aliyeondolewa, Mohamed Bazoum, aachiliwe huru.