Duterte aridhia waasi wa kikundi cha Kiislam Ufilipino kujitawala

Rais Rodrigo Duterte

Serikali ya Ufilipino Ijumaa imeridhia viongozi wa waasi wa kikundi cha Kiislam kujitawala katika jimbo jipya la Kiislam kusini mwa Ufilipino.

Kikundi hicho kilikuwa kikipingana na majeshi ya serikali ya Ufilipino kwa miongo kadhaa ili kuweka utawala wao wenyewe, lakini pia sasa wamekabidhiwa jukumu la kutafuta amani na maisha bora kwa watu wao.

Katika sherehe rasmi, Rais Rodrigo Duterte alimuapisha kiongozi wa kundi hilo la Kiislamu, Murad Ebrahim, mkuu wa kundi kubwa kuliko yote la Waislam nchini humo, kuwa waziri mkuu wa mpito katika hafla iliyoacha athari ya kipekee huko Manila.

Hatua hiyo inafuatia kura ya maoni iliopigwa Januari na wanainchi wakiomba kuwepo mkoa huru wa Bangsamoro, ikiwa pia ni kilelele cha kufikia makubaliano ya amani kumaliza vita ambayo waasi walikuwa wanadai uhuru wao uliyosababisha watu 150,000 kuuawa tangu vita hivyo kuanza mwaka 1970.

Rais Duterte na Murad, kiongozi wa kundi la Moro Islamic Front, wote kwa pamoja wamesema, wana imani makubaliano hayo yaliyofikiwa yatasaidia kuzuia kuongezeka kwa vikundi vya kiislam vyenye siasa kali katika mkoa wa kusini mwa Mindanao wenye Waislam wengi nchini humo.

Kubwa kuliko yote tunapenda kuona mwisho wa vita ambavyo vimeuangamiza mji wa Mindanao na kugharimu maisha ya watu wengi bila ya sababu yoyote,” Rais amesema.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.