Jamii ya kimataifa inatazama kwa makini wakati Donald Trump akikutana kwa mara ya kwanza tangu kuwa rais na kiongozi ambaye anadhaniwa kuwa mpinzani wake mkuu wa taji la mtu mwenye nguvu zaidi duniani – Rais wa Russia, Vladmir Putin.
Mkutano huo uliotarajiwa kufanyika ljumaa jioni, ulionekana kuangaziwa Zaidi kuliko suala jingine lolote kwenye mkutano wa siku mbili mjini Hamburg, Ujerumani, unaohudhuriwa na viongozi wa mataifa 20 yenye uchumi mkubwa duniani.
Trump, ambaye utawala wake bado ni mchanga na hana ujuzi katika nyanja ya diplomasia ya kimataifa, anakutana na mtu ambaye ni mjanja, aliyeingia mamlakani mnamo miaka 17 iliyopita kwa kile kilichoonekana kuwa mapinduzi ya Kremlin, na ambaye ana historia ya kuwasukuma sana watu anaojadiliana nao.
Russia imekuwa ikishutumiwa kwamba iliingilia kwa njia isiyo halali uchaguzi wa Marekani wa mwaka wa 2016. Hata hivyo, Putin amekanusha tuhuma hizo, huku Trump akionekana kutolipatia umuhimu mkubwa suala hilo.
Siku ya Alhamisi, Trump alisema inaonekana Russia ilihusika kwa kuingilia uchaguzi wa Marekani lakini akaongeza kwamab huenda nchi zingine pia zilihusika.
Trump pia amekuwa akiishinikiza Russia kusitisha uungaji mkono wa nchi ambazo zinashutumiwa kudhamini ugaidi.
Uhusuiano wa kidiplomasia kati ya Marekani na Russia ulionekana kuzorota zaidi wakati wa utawala wa rais Barack Obama.